KATIBU MKUU-OFISI YA WAZIRI MKUU ATOA MAAGIZO SITA KWA WATAKAOSHIRIKI TATHMINI ASDP II
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu wa Shughuli za Serikali Dkt. Jim Yonazi ametoa maagizo sita kwa Wadau, Timu ya wataalamu na Wataalamu Elekezi watakaoshiriki zoezi la Tathmini ya Nusu Muhula wa Utekelezaji wa Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDP II) pamoja na Uandaaji upya Mpango wa miaka mingine mitano, ili kuhakikisha zoezi hilo linaleta tija katika Programu na Sekta ya Kilimo kwa ujumla.
“Ili kuwa na tija katika Tathmini hii napenda kukumbusha na kusisitiza Wataalam Elekezi kuzingatia Mpango Kazi ili kukamilisha kazi kwa wakati, Wataalam Elekezi kutumia taarifa na kutoa tafsiri sahihi ya uchambuzi, Timu ya Wataalam kushiriki kikamilifu katika zoezi la Tathmini na kutoa ushirikiano wa kutosha pamoja na taarifa kwa Wataalam Elekezi pale itakapohitajika, Wizara za kisekta kutoa ushirikiano wa kutosha ikiwa ni pamoja na taarifa zitakazohitajika, Wataalam Elekezi kwa kushirikiana na wadau kuainisha mikakati itakayowezesha kutatua changamoto zilizojitokeza katika awamu ya pili ya utekelezaji wa Programu na Wadau wa Maendeleo na Sekta Binafsi kuendelea kuunga mkono zoezi hili kwa kutoa rasilimali fedha, utaalam na taarifa”, ndivyo alivyoagiza Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dkt. Jim Yonazi.
Dkt. Yonazi alitoa maagizo hayo Agosti 15, 2023 Protea Courtyard hotel, jijini Dar es salaam alipohutubia kama mgeni rasmi kufungua Kikao cha Awali cha wadau kujiandaa kwa zoezi la Tathmini ya Nusu Muhula- ambayo ni miaka mitano iliyokamilika ya utekelezaji wa (ASDFP II) pamoja na zoezi la kuandaa upya Mpango wa Utekelezaji wa Programu hiyo kwa miaka mitano iliyobaki. ASDPII ni Programu inayokelezwa kwa miaka 10 katika awamu mbili kila moja miaka mitano, ilizinduliwa tarehe 6 Juni, 2017/18- utekelezaji ulipoanza ambapo sasa uko katika nusu muhula ambayo ni miaka mitano, inayofanyiwa Tathmini na utekelezaji wa miaka 10 utakamilika mwaka 2027/2028.
Aidha, Katibu Mkuu Dkt. Yonazi aliwahakikishia wadau wote wa Sekta ya Kilimo katika mkutano huo kuwa Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu ambayo ni Mratibu Mkuu wa ASDP II itatoa ushirikiano wa kutosha kwa Wadau wote wakiwemo wale wa Maendeleo katika kuratibu na kusimamia mapitio ya Programu pamoja na mipango mikakati ya miaka mingine mitano ya kumalizia awamu ya pili ya utekelezaji wa ASDP II.
“Napenda kuwahakikishia kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu-Mratibu wa ASDP II na Serikali kwa ujumla itatoa ushirikiano wa kutosha kwa Wadau wa Maendeleo wakiwemo Alliance for Green Revolution in Africa – AGRA katika kuratibu na kusimamia mapitio ya Programu ya ASDP II pamoja na mipango mikakati ya kumalizia awamu ya pili ya miaka mitano ya utekelezaji”, alisema Dkt Yonazi
Pia aliwapongeza wadau mbalimbali wanaoendelea kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuyafikia malengo yake likiwemo Shirika la Kilimo na Chakula Duniani (FAO) pamoja na AGRA akisema ni washirika muhimu wa Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na wizara za sekta ya kilimo katika kuendeleza Sekta ya Kilimo nchini.
“Ni matumaini yangu kuwa ushikiano huu na wadau wengine utaendelea kuongezeka wakati wa kutekeleza yaliyomo kwenye Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili -ASDP II kwa miaka mitano ijayo 2023 –2028”, alisema Dkt Yonazi.
Wakati huohuo, Dkt Yonazi alitumia nafasi hiyo kuhitimisha hotuba yake kwa kuwakumbusha na kuwasihi wadau wote katika Sekta ya Kilimo kujisajili kushiriki mkutano wa Africa Food Systems Forum utafanyika nchini mapema mwezi ujao wa Septemba mwaka huu 2023 ambapo unatarajiwa kufanyika katika Kituo cha mikutano cha kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es Salaam na kukutanisha wadau mbalimbali kutoka ndani na nje ya Tanzania.
“Napenda kuwakumbusha kuwa Mkutano wa Africa Food Systems Forum utafanyika Tanzania mwezi Septemba, kuanzia tarehe 5-8, 2023. Serikali ya Tanzania mwaka huu ndiyo mwenyeji wa Jukwaa hilo la Mifumo ya Chakula Barani Afrika. Naomba wote tujisajili kushiriki ili kutumia fursa hiyo ipasavyo”, alihimiza Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu wa shughuli za Serikali) Dkt. Jim Yonazi.