Mradi wa Kuendeleza Kilimo na Uvuvi kutatua changamoto za ufugaji Viumbemaji Chato.

Mradi wa Kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP) unaofadhiliwa na shirika la Kimataifa la Kuendeleza Kilimo (IFAD) utaweza kwa kiasi kikubwa kusaidia kutatua baadhi ya changamoto wanazokutana nazo na kuwakwamisha wafugaji wa Viumbemaji katika kituo cha Rubambagwe kilichopo wilayani Chato, mkoani Geita.

Mkurugenzi wa Ukuzaji Viumbemaji kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Nazaeli Madala alisema hayo Mei 12, 2023 na kufafanua kuwa kituo cha Rubambagwe kipo katika hatua za ujenzi ambapo, nia na madhuni ya kituo ni kuhamasisha, kuendeleza na kusimamia ukuzaji viumbemaji kwa maana ya ufugaji wa samaki katika mabwawa na vizimba kwenye ukanda wa ziwa Victoria.

Dkt. Madala aliongeza kusema kuwa kituo hicho cha Rubambagwe pia kitatoa mafunzo ya utengenezaji wa chakula cha samaki, ufugaji na ulishaji sahihi kwa samaki ambapo wafugaji watafundishwa namna ya kutengeneza chakula cha samaki kwa kutumia malighafi za asili. Aidha alisema chuoni hapo kutakuwa na majengo yatakayowezesha wafugaji wanaotoka mbali kukaa hapo wakati wa mafunzo na kutakuwa pia na kiwanda kidogo cha kutengeneza chakula cha samaki.

Zaidi, Mkurugenzi Madala alisema kituo cha Rubambagwe kitazalisha vifaranga vya samaki ili kusaidia kutatua changamotoza ambazo wafugaji wanakutana nazo. "Kutakuwa na kitotoleshi ambacho kitakuwa na uwezo mkubwa wa kuzalisha vifaranga ambavyo vitakwenda kuwezesha vitotoleshi vya sekta binafsi kupata wazazi ", alifafanua

Akiongea na ujumbe kutoka Mradi huo uliotembelea kituo, mmoja wa wafugaji wa samaki katika kituo hicho cha Rubambagwe, mkoai Chato alibainisha changamoto mbili kubwa walizonazo wakisubiri mradi huu kukamilika kuwa ni uhaba na ugumu wa upatikanaji wa mbegu na chakula cha kulisha samaki.

Awali, ujumbe wa IFAD ulifika ofisini kwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita Prof. Godius Kahyarara ambaye alisema ujumbe huo umefika kwa wakati muafaka ambao wakazi wa mkoa wa Geita wanapaswa kuutumia sasa kujikita katika shughuli za kilimo na ufugaji wa viumbemaji na kuwekeza kwa uhakika katika sekta hizo kama wanavyowekeza katika sekta ya madini.

Ujumbe kutoka IFAD, wataalam na Mratibu wa Programu ya AFDP kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu- Sera Bunge na Uratibu Bw. Salim Mwinjaka, wamekuwa kwa siku kadhaa katika ziara ya ufuatiliaji na ukaguzi wa maeneo yanayotekelezwa mradi huo wa Kuendeleza Kilimo na Uvuvi.

  • Google+
  • E-mail
  • PrintFriendly