News & Events

Viongozi Simamiea kwa Weledi Utekelezaji wa Programu ya Kuendeleza Kilimo na Uvuvi-Dkt. Yonazi

KATIBU Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi amewataka watendaji katika mikoa, wilaya na halmashauri kote nchini kuhakikisha wanasimamia vyema na kwa weledi utekelezaji wa Programu ya Kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP) katika maeneo yao kwani ni sekta muhimu katika kuchangia ukuaji wa uchumi na usalama wa chakula nchini na duniani kote.

Dkt. Yonazi aliyasema hayo Mei 4, 2023, Jijini Dodoma, katika warsha ya Utambulisho na Uelewa wa Programu hiyo ya Kuendeleza Kilimo na Uvuvi kwa wadau, wakiwemo watendaji katika mikoa, wilaya na halmashauri nchini 

Katika warsha hiyo Katibu Mkuu Dkt. Yonazi aliwaambia wadau kuwa serikali imeona kuna ulazima wa kuwepo kwa usalama wa mbegu katika kilimo hivyo kupitia Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA) nchini, serikali imewekeza mbegu kwa wingi ili kuhakikisha inayafikia maono yake.

“Serikali imeona umuhimu na imeendelea kusimamia uzalishaji na upatikanaji wa mbegu bora ambapo hadi kufikia Aprili 2023, jumla ya tani 49,962.35 za mbegu bora zimepatikana sawa na asilimia 26.68 ya mahitaji ya tani 187,197 kwa mwaka”, alisema Dkt. Yonazi na kuongeza: "serikali imeweka jitihada na nguvu katika upatikanaji wa mbegu hizo ili kuhakikisha uwepo wa usalama wa chakula nchini ambapo kwa upande wa sekta ya uvuvi  serikali imehakikisha kunakuwa na manufaa  katika matumizi ya rasilimali zilizopo  ambazo zimekuwa  hazijatumika vizuri”.

Aidha Katibu Mkuu Dkt. Yonazi alisema serikali ina mpango wa kununua meli zitakazotumika katika kuvua samaki kwenye kina kirefu cha bahari ili kuwezesha upatikanaji samaki wa uhakika na kwa wingi, hivyo kuchangia katika kuongeza lishe kwa wananchi pia nchi kuzidi kunufaiika na rasilimali za uvuvi katika kukuza uchumi. 

Dkt Yonazi alifafanua kuwa, Programu ya AFDP pia itahusisha ujenzi, upanuzi na ukarabati wa miundombinu mingine ikiwa ni pamoja na upanuzi wa vituo vya uzalishaji wa vifaranga vya samaki kikiwemo cha Kingolwira mkoani Morogoro.

“Lazima tushirikishe wadau ili tupeleke elimu ya kuweza kuzalisha vifaranga na kujenga mabwawa, natoa msisitizo kwa viongozi wa mkoa na ngazi zote kuwa kuna jukumu la usimamizi, tuhakikishe tunasimamia mradi huu vizuri na kwa weledi, kushauri na kuutekeleza kwa wakati”, alisisitiza Dkt. Yonazi

Awali, akiongea wakati wa ufunguzi wa warsha hiyo Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Uratibu wa shughuli za Serikali kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu -Sera Bunge na Uratibu, Bw. Paul Sangawe alisema lengo la Programu hiyo ya Kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP) hususani kwa upande wa sekta ya uvuvi, ni kuendeleza ufugaji wa viumbe maji pamoja na kuanza uvuvi katika bahari kuu.

“Tunatazamia katika Program hii ya AFDP, meli zitanunuliwa kwa matumizi ya pande zote mbili za muungano wa  nchi yetu na kuwezesha kwa mara ya kwanza nchi yetu kufanya uvuvi katika bahari kuu ili kuweza kutumia rasilimali tulizonazo kwa  uhakika na ufasaha’’, alisema Mkurugenzi Sangawe na kuongeza kusisitiza:  ‘’Pia kuhakikisha uzalishaji wa mbegu pamoja na usambazaji, na kuhakikisha fedha za mkopo ambazo tumepewa kutoka Mfuko wa Kimataifa wa Kuendeleza Kilimo  (IFAD) takribani dola 58.8 milioni, zinatumika kwa ufanisi na kuleta tija katika utelezaji wa Program hii”.

Naye  mwakilishi wa Mkurugenzi wa Uchumi na Uzalishaji toka Ofisi ya Rais -TAMISEMI, Afisa Kilimo Mkuu Dkt. Rehema Mdendemi alisema Programu hii ya AFDP ya Kuendeleza Kilimo na Uvuvi ni ya muhimu kwa serikali na wanachi kwa ujumla kwani itasaidia katika kuboresha maisha ya wakulima na wavuvi nchini na kuwaweka wananchi salama kwa kujitosheleza kwa chakula pia kuleta ajira kwa watu wengi hususani vijana.

  • Google+
  • E-mail
  • PrintFriendly