Waziri Mkuu, aagiza ukamilishaji wa utoaji wa mitambo ya ujenzi kiwanda cha sukari Mbigiri
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametoa agizo kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Mwigulu Nchemba na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Tixon Nzunda kukutana ili wakamilishe taratibu za utoaji wa mitambo ya ujenzi wa kiwanda cha Sukari cha Mbigiri kilichopo wilayani Kilosa.
Agizo hilo limetolewa Agosti 14, 2021 baada ya kupokea taarifa ya ujenzi wa kiwanda hicho, wakati alipotembelea mradi wa shamba la miwa la Mkulazi pamoja na kukagua bwawa la umwagiliaji, pump house pamoja na ujenzi wa kiwanda cha sukari Mbigiri, mkoani Morogoro ambapo katika taarifa hiyo Waziri Mkuu alielezwa kuwa kuna baadhi ya mitambo ya ujenzi wa kiwanda imekwama bandarini.
“Tunataka kiwanda hiki kianze kujengwa, ucheleweshwaji usio na umuhimu hauna nafasi, hatutaki ujenzi ukwame, zile kontena 21 kule bandarini tunahitaji zitoke Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Waziri wa Fedha na Mipango na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu mkae mkokotoe kile kinachopaswa kulipwa kijulikane mitambo ile itoke.” Waziri Mkuu alisema.
Aidha amesema kwa namna nchi ilivyojipanga katika ujenzi wa viwanda, Tanzania itakuwa na viwanda saba vya sukari lengo likiwa ni kuhakikisha inajitosheleza kwa kuwa na sukari ya kutosha na kuondoa pengo la tani 70,000 lililopo, hivyo kupunguza uagizaji wa bidhaa hiyo kutoka nje ya nchi.
Mbali na maagizo hayo, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuipongeza Bodi ya Mkulazi, watendaji wa shamba la Miwa la Mkulazi pamoja na uongozi wa kiwanda cha Sukari cha Mbigiri kwa usimamizi mzuri wa mradi huo kutokana na hatua kubwa ya maendeleo iliyofikiwa.
Kwa upande wake mbunge wa jimbo la Mikumi Mh. Dennis Londo amemshkuru Waziri Mkuu kwa niaba ya Serikali kwa namna ambavyo imekuwa ikiontesha jitihada katika zao la miwa ikiwemo utatuzi wa changamoto mbalimbali kwani zao hilo limekuwa na mafanikio na kwa wilaya ya Kilosa sio ni zao la kilimo bali ni uchumi na maisha.