News & Events

ASDP II ITALETA MAGEUZI KATIKA SEKTA YA KILIMO NCHINI-DKT TIZEBA

Mhe Mhandisi Dkt Charles Tizeba (Mb) Waziri wa kilimo, ameitaja Programu ya kuendeleza sekta ya kilimo awamu ya pili (Agricultural sector Development Programme ASDP II) kwamba italeta mageuzi makubwa katika sekta hiyo zikiwemo sekta zingine ya Mifugo na Uvuvi kwa kuongeza uzalishaji, tija na kufanya kuwa na matokeo makubwa yatakayopelekea kupungua kwa madhara ya mabadiliko ya tabia nchi.

Dkt Tizeba ameyasema hayo Leo tarehe 19 Septemba 2018 wakati wa uzinduzi wa Mradi wa utafiti na kujenga uwezo wa kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi katika nyanja za kilimo na mfumo wa chakula nchini Tanzania hafla iliyofanyika katika ukumbi wa ESRF Jijini Dar es salaam.

Alisema kuwa ASDP II ni Programu ya miaka 10 itakayotekelezwa kuanzia mwaka wa 2017/2018 hadi 2027/2028 katika vipindi viwili vya miaka mitano mitano. Awamu ya kwanza itaanza kutekelezwa 2017/2018 hadi 2022/2023 ambayo ni muendelezo wa awamu ya kwanza ya ASDP 1 iliyotekelezwa kuanzia mwaka 2006/2007 hadi 2013/2014.

Alieleza kuwa Programu hiyo imezingatia malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2025, Mpango wa Maendeleo wa muda mrefu 2012-2021, Mpango wa Maendeleo wa miaka mitano 2016-2021, Mkakati wa kuendeleza sekta ya kilimo 2015 na Mpango wa uwekezaji katika kilimo na lishe (Tanzania Agriculture and Food Security Investment Plan -TAFSIP 2011). 

Pia alisema kuwa Wizara ya kilimo inaendelea kukuza na kulinda Maendeleo ya sekta ya kilimo yaliyo endleevu kwa kuongeza uzalishaji, kubiresha mifumo inayokwenda sambamba na tabia nchi kwa kuzingatia mabadiliko ya tabia ya nchi kwa umakini mkubwa sana kwani Tanzania ni miongoni mwa nchi chache ambazo zimefanikiwa kuendeleza Mpango mkakati wa kupambana na mabadiliko ya tabia ya nchi ili kwenda sambamba na Dira ya maendeleo ya Taifa 2025. 

Alisema kuwa serikali inatambua juhudi zitakazotolewa na mradi wa utafiti wa kujenga uwezo wa kukabiliana na mabadiliko ya Tabia ya nchi katika nyanja za kilimo na Mfumo wa chakula nchini Tanzania CCRF-AFRICAP katika kuelewa mustakabali wa sekta ya kilimo.

Mradi huo wa CCRF-AFRICAP ni mradi wa kikanda utakaojumuisha nchi nne Barani Afrika ambazo ni Tanzania, Malawi, Afrika kusini, na Zambia ambapo kwa upande wa Tanzania Mradi huo utasimamiwa na ESRF ambazo ni wawakilishi wa mtandao wa Taasisi zinazojihusisha na uchambuzi wa sera katika nyanja za chakula, kilimo, na maliasili Barani Afrika (FANRPAN) ukijumuisha watafiti katika nyanja za mifumo ya kilimo ikiwemo sayansi ya udongo, sayansi ya mimea, sayansi ya Mifugo na ikolojia, kisiasa na sayansi ya jamii.

Kwa mujibu wa Dkt Tausi Mbaga Kida, Mkurugenzi wa Taasisi ya tafiti za kiuchumi na kijamii ESRF, alisema kuwa lengo la mradi huo ni kuainisha na kutekeleza Sera zinazotokana na uthibitisho wa kisayansi kupitia utafiti katika kuendeleza Maendeleo endelevu, uzalishaji, mifumo ya kilimo inayozingatia mabadiliko ya tabia nchi ili kuwezesha kufikia usalama wa chakula na Maendeleo ya kiuchumi.

Mabadiliko ya tabia nchi ni miongoni mwa changamoto inayoikabili mataifa ya Afrika katika karne ya 21 kwani inakadiriwa kuwa idadi ya watu watakaokuwa hatarini kwa njaa itaongezeka maradufu Barani Afrika pia kupelekea ongezeko la ukame , kupungua kwa uzalishaji na kubadilika kwa Nyakati za hali ya hewa yatakayopelekea kupungua kwa uzalishaji wa Mazao mengi ya chakula yanayostawi sana.

  • Google+
  • E-mail
  • PrintFriendly