News & Events

Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo-ASDP II imeleta mafanikio katika kukuza Uchumi-Dkt Yonazi

SERIKALI itaendelea kuweka kipaumbele katika kuendeleza Sekta ya Kilimo nchini kwa kuwa ni sekta muhimu na yenye tija katika uhakika wa chakula, kukuza uchumi na maendeleo kwa Taifa.

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu wa shughuli za serikali Dkt. Jim Yonazi alitoa kauli hiyo Agosti 15, 2023 jijini Dar es salaam alipohutubia kufungua Kikao cha Awali cha Wadau kujiandaa kwa zoezi la Tathmini ya Nusu Muhula ambayo ni miaka mitano ya utekelezaji wa Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDP II) pamoja na Uandaaji upya Mpango wa Utekelezaji wa Programu hiyo kwa miaka mitano iliyobaki na kuipongeza Programu kuwa imefanikiwa kujenga uwezo katika kilimo na hivyo kuleta mafanikio katika kukuza uchumi wa nchi. 

Programu ya ASDP II inatekelezwa kwa miaka 10 katika awamu mbili kila moja miaka mitano, ilizinduliwa Juni 6 mwaka 2017/18 na kiongozi mkuu wa nchi ambapo utekelezaji wake wa miaka 10 utakamilika 2027/2028. Malengo makuu ya ASDP II ni kuleta mageuzi katika Sekta ya Kilimo ambayo inajumuisha kilimo cha mazao, mifugo na uvuvi pamoja na mazao ya nyuki, ili kuongeza uzalishaji na tija, kukifanya kilimo kiwe cha kibishara zaidi na kuongeza kipato cha wakulima wadogo na wa kati kwa ajili ya kuboresha maisha yao, kuongeza uhakika wa usalama wa chakula na lishe na kuchangia kwenye pato la Taifa 

“Sekta ya kilimo ni muhimu uendelea kupewa kipaumbele na wadau wote kwa kuwa ni ya muhimu pia katika kukuza uchumi wa Taifa letu na tegemeo kwa maisha ya wananchi wengi. Sekta hii inaongoza kwa uchangiaji mkubwa katika pato la Taifa, na robo tatu ya bidhaa zinazouzwa nje ya nchi. Ni sekta ya chanzo cha chakula pamoja na utoaji wa fursa za ajira zaidi ya asilimia 75 ya watanzania na mwaka 2021 ilichangia asilimia 26.1 katika shughuli za kiuchumi katika Pato la Taifa.”, alisema Dkt Yonazi na kuendelea kufafanua kuwa ndio maana Tanzania  imeamua kuwa na uchumi wa kilimo ambao una faida na tija kwa  kuwa mafanikio katika sekta ya kilimo yatasaidia  nchi  kuendelea kwa haraka, kujitosheleza kwa chakula  na kuwa na nguvu za kiuchumi ambazo ni endelevu  kwa ajili ya  wananchi  wote.

Aidha Katibu Mkuu Dkt. Yonazi alisema, sekta ya Kilimo ni ya kipaumbele kwa nchi kwani  licha ya kuhitaji nguvu za pamoja kutoka Wadau, Sekta na Taasisi mbalimbali, ina uhusiano pia na sekta zisizo kuwa za kilimo kupitia usafishaji kwenda kwenye usindikaji wa mazao ya kilimo, matumizi na uuzaji mazao nchi za nje, malighafi kwa viwanda na soko kwa bidhaa zilizotengenezwa na kusisitiza kuwa “ni kwa msingi huo, Mheshimiwa Rais ameipa sekta ya Kilimo kipaumbele cha kipekee ambapo kwa miaka miwili mfululizo ameongeza bajeti kwa kiwango kikubwa”.

Katika hotuba yake, Dkt. Yonazi alibainisha kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu ambayo ni Mratibu Mkuu  wa shughuli za serikali  ina dhamana ya Uratibu wa Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDP II)  na kuhakikisha  inapata ushirikiano  wa  wadau wa sekta zote  za kilimo na zisizo za kilimo  kama vile sekta ya Usafirishaji,  Viwanda na Biashara  na zinginezo   ili iweze kusonga mbele katika utekelezaji  wake na kuleta tija na kwamba kwa kutambua umuhimu wa Programu hiyo na hatua iliyofikiwa katika utekelezaji, ndio maana kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, inaratibu zoezi la Tathmini ya Programu pamoja na uandaaji upya wa Mpango wa Programu katika kipindi kilichobaki cha miaka mitano kutoka sasa 2023 hadi 2028.  

“Tumedhamiria kuiendeleza Programu ya ASDP II na kuhakiisha inakuwa ya kutolewa shuhuda kwa mafanikio na kamwe isiingie wenye orodha ya Programu zisizotekelezeka. Lakini mafanikio hayo hayatawezekana kwa kupitia tu Ofisi ya Waziri Mkuu bali kwa ushiriiano na mshikamano na ninyi wadau wote ili tuweze kuwa na tija na kasi katika utekelezaji wa Programu hii” alisema Katibu Mkuu Dkt. Yonazi

Programu ya ASDP II ina maeneo makuu manne ya kipaumbele katika kuitekeleza ambayo ni pamoja na eneo la Usimamizi Endelevu wa Matumizi ya Maji na Ardhi lenye lengo la kuongeza wigo wa upatikanaji wa maji na matumizi bora ya ardhi kwenye kilimo, ufugaji na uvuvi. Eneo la pili ni  la kuongeza Tija na Faida  kwa lengo la kuongeza uzalishaji wenye tija hasa kwenye mazao ya kipaumbele, Eneo la tatu linahusu kuongeza Thamani ya Mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi ili kuleta ushindani  kwenye soko na sekta binafsi pamoja   na kuhakikisha uanzishwaji wa vyama vya wakulima, ambapo eneo la nne ni lile la kuweka Mazingira Wezeshi ya kuendeleza sekta ya Kilimo pamoja na kuwezesha Uratibu wa Programu, katika shughuli mbalimbali za  uhamasishaji, ufuatiliaji, na kufanya tathmini ya Sekta na kuimarisha Taasisi.

“Najua kuwa Tathmini ya ASDP II itaainisha mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka mitano ya utekelezaji. Na nyote mnajua kuwa tumepata mafanikio makubwa katika utekelezaji wa Programu hii”, alisema Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Dkt. Yonazi na kuendelea kubainisha mafanikio hayo kuwa ni pamoja na kuwapo Matumizi Endelevu ya Maji na Ardhi ambapo idadi ya vijiji vyenye matumizi bora ya ardhi imeongezeka mpaka 2,860 katika kuelekea malengo yaliyowekwa ya vijiji 3,800, kuongezeka kwa eneo la umwagiliaji hadi kufikia hekta 783,749 dhidi ya malengo ya hekta 763,120, kuongezeka kwa vyanzo vya maji kwa ajili ya mifugo kufikia 1,412 dhidi ya malengo yaliyowekwa ya vyanzo 2,076. 

Aliyataja mafanikio mengine kwenye sekta ya kilimo na kwa nchi  yaliyotokana na utekelezaji wa ASDP II kwa miaka mitano sasa kuwa ni kuongezeka kwa Tija na Faida katika kilimo ambapo imeongezeka kwenye mazao ya sukari, nyama na maziwa,  kujitosheleza kwa chakula kwa wastani wa asilimia 121 licha ya kwamba imekuwa wakati mwingine ikipungua mpaka asilimia 114 na hiyo bado ni ongezeko, pamoja na ongezeko la Thamani na Masokoambavyo vimepunguza  tofauti zilizokuwepo kati ya bei ya mazao shambani na bei ya sokoni katika mazao ya mahindi, mpunga, mtama na uwele, pamoja na kupungua kwa upotevu wa mazao baada ya mavuno katika mazao ya mahindi, mihogo na maziwa. 

Mafanikio mengine katika sekta ya kilimo yaliyotajwa kutokana na utekelezaji wa ASDP II ni kuwepo viwezeshi vya sekta, uratibu, uhamasishaji, ufuatiliaji na tathmini vilivyofanikisha kufanyika mapitio na maboresho ya sera na sheria mbalimbali zinazohusu mazao na mifugo, kufanikisha kuongezeka kwa uwekezaji mpya wa sekta binafsi kwenye mazao na mifugo na kufanikisha uwezeshaji wa vikundi vya wakulima wadogo.

Pamoja na mafanikio, Katibu Mkuu Dkt. Yonazi alisema kuwa Tathmini ya nusu muhula wa Utekelezaji wa ASDP II itaainisha pia changamoto zilizojitokeza wakati wa utekelezaji wa Program kwa miaka mitano ya awali  ili ziangaliwe kwa kina na kuwekewa mikakati na mipango  ya kuzitatua na kuzitumia kama fursa ili ASDP II izidi kusonga mbele na kuzitaja  baadhi ya changamoto  kuwa ni upatikanaji mdogo wa fedha za utekelezaji kwa kuzingatia bajeti na muundo wa Programu, kukua kwa uzalishaji unaochagizwa zaidi na ongezeko la eneo kuliko tija, kasi ndogo ya utekelezaji wa Programu ikilinganishwa na malengo, changamoto za fedha za uratibu, uhamasishaji,  ufuatiliaji na tathmini ya Programu,  pamoja na  kuzuka kwa UVIKO 19- hali iliyoathiri ufikiaji wa masoko ya nje na uingizaji nchini wa pembejeo kutoka  nje ya nchi pamoja na kupotea kwa nguvu kazi wenye sekta mbalimbali. 

Kuhusu uandaaji upya Mpango wa Utekelezaji Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDP II) kwa miaka mitano iliyobaki kuanzia 2023/24 hadi 2027/28,  Katibu Mkuu Dkt Yonazi alitoa maelekezo akisema kuwa, kama ilivyo katika mapitio ya Mipango na Mikakati mingine, mapitio na uhuishaji wa ASDP II yatahusisha uchambuzi wa nyaraka na maandiko mbalimbali yanayohusiana na maendeleo ya Sekta ya Kilimo nchini akisisitiza kuwa ”ni muhimu kila sekta kuhakikisha inatoa takwimu na taarifa sahihi na za kutosha ili kuwezesha Tathmini kuwa na uhalisia pamoja na kuwezesha Mpango utakaoandaliwa kutekelezeka kwa ufanisi”.

Aidha Katibu Mkuu Dkt. Yonazi alielekeza kuwa Wadau wa Maendeleo na Sekta Binafsi kama ilivyo kwa wadau wengine, watashirikishwa katika Tathmini na maandalizi ya Mpango mpya wa miaka mitano ya Utekelezaji wa ASDP II na kuwaambia “tunategemea mtatoa ushirikiano na taarifa muhimu zitakazowezesha zoezi hili kuwa na tija na manufaa kwa Taifa. Tunategemea pia kuwa taarifa mlizonazo kuhusu Mikakati mnayotekeleza katika maeneo yenu zitasaidia kuonesha namna mikakati hiyo ilivyowianishwa na kufungamanishwa na Programu ya ASDP II na maeneo ya kuboresha”.

Dkt. Yonazi aliongeza kusema “Ni kwa ushirikishwaji jumuishi tutaweza kupata picha halisi ya hatua tuliyofikia katika utekelezaji, changamoto na maeneo yanayohitaji kujipanga ili kufikia malengo ya Programu.Nina imani kuwa uhuishaji wa ASDP II utabeba uhalisia wa ufikiwaji malengo ya mageuzi kwenye   Sekta ya Kilimo kama inavyoonekana kwenye Agenda 10/30, mageuzi ya mifumo endelevu ya chakula na kadhalika”.

Awali alipoanza hotuba yake Katibu Mkuu Dkt Yonazi alishukuru Shirika la Alliance for Green Revolution in Africa–AGRA, kuwezesha Ofisi ya Waziri Mkuu kuratibu zoezi la mapitio ya utekelezaji wa Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDPII) kwa kipindi cha miaka mitano ya kwanza- 2018–2023 na zoezi la uandaaji wa Mpango wa miaka mitano ijayo litakalofuatia Tathmini. Pia alishukuru Shirika la Kilimo na Chakula Duniani (FAO) kwa kuunga mkono juhudi hizi ambapo wamewezesha kuwajengea uwezo timu ya wataalamu wa ndani itakayoshirikiana na mshauri mwelekezi katika zoezi hilo la Tathmini ambapo timu hiyo itakuwa na mchango mkubwa katika kutoa taarifa na maoni ambayo yatazingatiwa na Mshauri Mwelekezi kabla ya vikao vya wataalam na viongozi. Zaidi, aliwashukuru Makatibu Wakuu na wakuu wa Taasisi kuwapo kikaoni na kuruhusu wataalam wao kushiriki hadi mwisho wa zoezi la Tathmini ya Utekelezaji wa ASDP II kwa miaka mitano ya awali.

Alisema kama ilivyo muhimu kwa wadau wengine wote wa ASDP II, AGRA imekuwa pia  mshirika muhimu wa Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na Wizara za sekta ya Kilimo ambapo kupitia ushirikiano huo mambo kadhaa makubwa yamefanyika ikiwemo pia Tathmini Jumuishi ya Sekta ya Kilimo (Joint Agricultural Sector Review) Uhuishaji wa Mipango ya Kilimo ngazi za Halmashauri (DADPs), Uchambuzi wa kodi kwenye sekta ndogo ya mafuta ya kula na namna ya kuchochea uzalishaji wa mafuta ya kula nchini na Maandalizi ya andiko la Ajenda 10/30. 

“Ni matumaini yangu kuwa ushikiano huu na wadau wengine utaendelea kuongezeka wakati wa kutekeleza yaliyomo kwenye Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili kwa Miaka Mitano ijayo (2023 –2028)”, alisema Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi, na kufungua mkutano huo wa kujiandaa na Tathmini ya ASDP II wa siku moja, uliofanyika Protea Courtyard-Hotel, jijini Dar es salaam.

-#-

  • Google+
  • E-mail
  • PrintFriendly