News & Events

Dkt.Yonazi: Sekta ya Kilimo na Uvuvi ni Utajiri

KATIBU MKUU Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshugulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi amesema sekta ya kilimo na uvuvi ni utajiri kwa kuwa zina tija katika kuleta maendeleo ya taifa letu kwa kuzingatia fursa zilizopo.

Ametoa kauli hiyo wakati wa ziara yake ya kikazi kutembelea na kukagua utekelezaji wa miradi ya Kuendeleza sekta ya Kilimo na Uvuvi ya AFDP inayoratibiwa na ofisi yake Mkoani Morogoro.

Dkt. Yonazi alitembelea baadhi ya Wilaya zinazotekeleza mradi huo ikiwemo Morogoro Mjini na Kilosa ambapo alikagua utekelezaji huo katikaTaasisi ya Utafiti wa Mbegu (TIRA), Taaasisi ya Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA), Taasisi ya Udhibiti wa Ubora wa Mbegu (TOSCI) pamoja na Kituo cha Viumbe Maji (DAQ) kilichopo Kingolwira mkoani Morogoro.

Alifafanua kuwa nchi ya Tanzania ina utajiri mwingi kupitia fursa zinazotokana na sekta hizo za kilimo na uvuvi na kwamba nchi itakuwa kituo cha maarifa ya kujifunza kilimo na uvuvi kwa nchi za Afrika Mashariki kutokana na jitihada za Serikali katika kuwekeza katika sekta hizo.

Aliongezea kuwa kupitia mradi wa kuendeleza sekta ya kilimo na uvuvi ambao utasaidia kuendelea kuboresha miundombinu muhimu kwa lengo la kuhakikisha ufugaji unakuwa sehemu ya pato la taifa na kuchangia kasi ya maendeleo pamoja na kuliingizia taifa fedha za kigeni.

“Tanzania imeendelea kuwekeza katika sekta ya uvuvi na kilimo, na hii itaipa nafasi nchi yetu kuwa kituo cha maarifa ya kujifunza masuala ya kilimo na nchi zinazotuzunguka, ni muda sahihi kuendelea kuweka nguvu zaidi kwa kuzingatia mazingira yetu ya uwekezaji”, alisema Dkt. Yonazi.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Fatma Mwassa alipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kuleta miradi hiyo katika mkoa wake huku akiitaja Morogoro kwa mafanikio makubwa eneo la kilimo na uvuvi kwa kuzingatia ardhi yenye rutuba kwa mkoa wa Morogoro.

“Mkoa wetu una mvua nyingi na umeendelea kuwa mzalishaji mzuri wa mazao ikiwemo mpunga. Tumeendelea kuwa wa kwanza kwa uzalishaji wa mpunga nchini, namba sita kwa uzalishaji wa ndizi, namba nne kwenye G5 katika uzalishaji wa chakula nchini, malengo yetu ni kufanya vizuri zaidi ili kusogea kutoka nafasi ya nne kitaifa na kuwa nafasi nzuri zaidi,” alisema mkuu wa mkoa Bibi Mwassa.

Aliongezea kuwa, mkoa wake wa Morogoro umeendelea kutoa kipaumbele katika masuala ya kilimo kwa kuendelea kutenga bajeti.

Awali akieleza lengo la mradi wa AFDP, Mratibu wa program hiyo kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Salimu Mwijaka alisema, hadi sasa mradi umeifikia mikoa 11 ambayo ni Morogoro, Geita, Lindi, Tanga, Pwani, Dodoma, Singida, Manyara,Tabora, Geita, Shinyanga na Mwanza na kuongeza kuwa umejipanga kufanya vizuri kwa matokeo yenye tija.

“Mradi huu umejikita katika maboresho maeneo mengi ikiwemo ya kuboresha mtandao wa usambazaji mbegu, na kuhakiksiha tunaboresha maeneo ya umwagiliaji, upatikanaji wa vifaa kama matrekta katika mashamba, udhibiti wa mbegu katika maabara. Aidha  kwa upande wa samaki tumeendelea kujenga na kuongeza uwezo wa vitotoreshi vya vifaranga vya samaki, kuboresha mabwawa ya kufugia samaki,“alisema Bw. Mwijaka

Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Kituo cha Ukuzaji viumbe Maji cha Kingolwira Bi.Gillness silayo alieleza faida za program ambayo utaleta unafuu kwa kutatua changamoto wanazokabiliana nazo ikiwemo uchakavu wa mabwawa na ukosefu wa maji.

“Mradi wa IFAD utatusaidia kuboresha mabwawa yetu 20, hivyo kuongeza makusanyo ya maduhuri, pamoja na hilo mradi utatuchimbia visima vitavyotatuta changamoto ya maji katika ufugaji wa samaki,” alisema Bi Gillness.

  • Google+
  • E-mail
  • PrintFriendly