Mifugo Elfu 25 kuanza kuvishwa Hereni za utambuzi wa kieleroniki Arusha DC
Na. Elinipa Lupembe
Halmashauri ya Arusha inategemea kuanza rasmi zoezi la utambuzi wa mifugo elfu 25 kwa awamu ya kwanza, ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Serikali laa kivisha mifugo hereni za kielekroniki, lengo kubwa likiwa ni utambuzi wa mifugo kuanzia umiliki wake pamoja na eneo inapotokea mifugo hiyo.
Akizungumza wakati wa kupokea hereni hizo kutoka kampuni ya S&J Daktari wa Mifugo halmashauri ya Arusha, Dkt. Yohana Kiwone amethibitihsa kupokea jumla ya hereni elfu 25, kutoka kwa Kampuni hiyo, tayari kwa kuanza zoezi la uvishaji hereni za utambuzi mifugo katika halmashauri ya Arusha.
Dkt. Kiwone amesema kuwa, katika halmasahuri ya Arusha, zoezi la utambuzi litafanyika kwa awamu 4, ambapo jumla ya mifugo 200,019, inategemea kuvikwa hereni hizo za kielektoniki, ng'ombe 81,550, punda 3,535, mbuzi 60,671 na kondoo 54, 245, huku awamu ya kwanza ikitegemea kuvikwa jumla ya mifugo elfu 25.
Aidha Dkt. Kiwone amewataka wafugaji wote wa halmashauri ya Arusha, kuwa tayari kutekeleza agizo hilo ka serikali la kuvika mifugo yao hereni za Kielektroniki, na kuainisha mifugo ambayo itavikwa hereni hizo ni pamoja na ng'ombe, mbuzi, kondoo na punda.
"Kila mfugaji atagharamia hereni kwa mifugo yake, bei ya ng'ombe na punda ni shilingi 1,750 na bei ya mbuzi na kondoo itakuwa shilingi 1,000 kwa kila mfugo mmoja, hivyo wafugaji wote wanapaswa kujitokeza wakati wa zoezi hilo katika maeneo yao" amefafanua Dkt. Kiwone.
Hata hivyo amezitaja faida za uwekaji hereni hizo za kielekroniki ni pamoja na kutambua mifugo kulingana na umiliki na eneo inapotokea, kidhibiti wizi wa mifugo na magonjwa, kuimarisha soko la ndani na nje la bidhaa za mifugo pamoja na kutatua changamoto ya migogoro baina ya wakulima na wafugaji inayojitokeza mara kwa mara nchini.
Awali utambuzi wa mifugo kwa njia ya kielektroniki unafanyika kwa mujibu wa sheria Na 12 ya utambuzi, usajili na ufuatiliaji ya mwaka 2010, inayoelekeza kutumia hereni za kielektroniki na taarifa za mifugo na mfugaji zitachukuliwa kwenye nakala ngumu na nakala za kielekitroniki na kuingizwa kwenye kanzu data ya Taifa.