Programu ya AFDP kuchochea maendeleo sekta ya Kilimo na Uvuvi

KATIBU MKUU Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi amesema Serikali imedhamiria kuendelea kuwekeza katika sekta ya Kilimo na Uvuvi kwa lengo la kuchagiza maendeleo kupitia miradi inayotekelezwa na programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo na Uvuvi ya AFDP nchini.

Ametoa kauli hiyo wakati wa ziara yake ya kikazi katika Wilaya ya Morogoro Mjini na Kilosa Mkoani Morogoro, alipotembelea na kukagua shughuli za utekelezaji wa programu hiyo inayoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu.

Katika ziara yake ametembelea Taasisi za Wakala wa Mbegu za kilimo (ASA),Taasisi ya utafiti wa Mbegu (TARI), Taasisi ya udhibiti Ubora wa Mbegu (TOSCI) pamoja na kukagua kituo Cha Viumbe Maji (DAQ) Kingolwira ikiwa ni sehemu ya maeneo yanayotekelezwa na program hiyo.

Dkt. Yonazi alisema uwekezaji huo utachangia kuongeza uzalishaji katika kilimo na uvuvi hivyo kuchangia ukuaji wa uchumi wa nchi na kuifanya kuwa na chakula cha kutosha

Aliongezea kuwa uwekezaji huo pia utawasaidia wananchi kuendelea kujifunza katika maeneo yanayotekeleza miradi hii hivyo kujiletea maendeleo yao.

“Maeneo yanayotekelezwa miradi ya AFDP yataleta chachu kwa wananchi kujifunza na kujipatia maarifa yatakayowasaidia kujikwamua kiuchumi, hivyo itumieni miradi hii kama fursa ya kipekee”, alisema Katibu Mkuu Yonazi.

Naye Mtendaji Mkuu Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA) Dkt. Sophia Kashenge alisema kwa kuwa Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu imeendelea kuongeza tija katika kuendeleza sekta ya kilimo na uvuvi kupitia miradi mbalimbali, ni dhahiri wao ASA wataendela kuunga mkono jitihada hizo kwa vitendo huku akibainisha  mafanikio yaliyofikiwa na taasisi yake.

“Tumejipanga kuhakikisha tunaendelea kuwekeza katika sekta ya kilimo mafanikio yatokanayo na sekta hii, ASA itaendelea kuwa na mbegu bora zenye kukidhi mahitaji yaliyopo”, alisema Dkt. Sophia

  • Google+
  • E-mail
  • PrintFriendly