News & Events

WAKULIMA LIMENI ALIZETI MPATE FAIDA YA HARAKA – WAZIRI MKUU MAJALIWA

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa mchana wa leo tarehe 13 Juni, 2021 amewaasa Wakulima wa mikoa inayolima alizeti kujikita kwenye kilimo cha zao hilo kwa kuwa katika kipindi kifupi wanaweza kupata faida kubwa kwa kuwa mahitaji ya zao hilo ndani na nje ya nchi ni makubwa.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa ameyasema hayo wakati akiongoza mkutano mkubwa wa Wadau wa zao la alizeti mkoani Singida katika ukumbi wa Kituo cha Kanisa Katoliki na kusisitiza kuwa kilimo cha alizeti kinachukua muda mfupi wa miezi minne tu kuanzia wakati wa kupanda hadi kuvuna.

Waziri Mkuu Majaliwa amesema kwenye kilimo cha zao la alizeti kuna fursa kubwa ambayo inapswa kuchangamkiwa na Wakulima wa mikoa ya Singida, Simiyu, Manyara, Tabora na kuongeza kuwa Uzalishaji wa mafuta ya kula nchini mdogo ambapo ni tani 290,000 tu ambazo uzalishwa nchini; Kiasi hicho ni sawa na asilimia 45 ya mahitaji ya mafuta ya kula ambayo ni tani 650,000 kwa mwaka.

“Nchi huagiza tani zipatazo 400,000 kufidia upungufu wa mafuta ya kula na hugharimu zaidi ya Shilingi bilioni 474 kwa mwaka kwa takwimu za sasa”. Amekaririwa Waziri Mkuu Majaliwa.

Mbali na hamasa hiyo Waziri Mkuu Majaliwa amesema kutokana na umuhimu wa mafuta ya kula, Serikali imeweka mkakati wa kuongeza uzalishaji wa mazao ya mafuta yakiwemo chikichiki, alizeti, pamba, karanga na ufuta ili kujitosheleza na kuondokana na uagizaji wa mafuta kutoka nje ya nchi. 

Waziri Mkuu Majaliwa amesema hatua za awali ya kutekeleza mikakati ya kuendeleza zao la michikichi kwa kuweka nguvu katika mkoa wa Kigoma ambapo Serikali iliamua kuanzisha Kituo maalum cha utafiti wa mchikichi cha Kihinga. Kupitia utafiti huo, matokeo makubwa ya uzalishaji wa miche bora yenye uwezo wa kuzalisha mafuta kiasi cha wastani wa tani 5 kwa hekta yameanza kuonekana ikilinganishwa na aina ya michikichi ya zamani iliyopo sasa inayozalisha wastani wa mafuta ya mawese tani 1.6 kwa hekta.

“Ninapenda kuwajulisha kuwa hadi kufikia Mei, 2021 jumla ya mbegu 5,630,376 za chikichi na miche milioni 1.5 imezalishwa na kusambazwa katika Mikoa ya Kigoma, Katavi, Kagera, Rukwa, Mbeya, Pwani na Ruvuma.”Amesisitiza Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Waziri Mkuu Majaliwa amesema mkutano wa Singida una lengo la kujadiliana kuhusu changamoto zinazoikumba Sekta ya Kilimo kupitia zao la alizeti.

“Tumekutana hapa leo kwa lengo la kujadili changamoto na fursa mbalimbali zinazoikabili Tasnia ya Alizeti ili kuja na mikakati madhubuti itakayochangia kuongeza uzalishaji na tija hivyo kuwa na uhakika wa upatikanaji wa mafuta ya kula nchini.”

“Katika mwaka 2019/2020 uzalishaji wa alizeti nchini umefikia tani 649,437 ikilinganishwa na tani 561,297 kwa mwaka 2018/2019. Pamoja na ongezeko la uzalishaji wa mazao ya mafuta nchini bado kuna changamoto mbalimbali zinazohitaji kupatiwa ufumbuzi.” Amekaririwa Waziri Mkuu Majaliwa.

Waziri Mkuu Majaliwa amezitaja changamoto hizo kuwa ni pamoja na tija ndogo katika uzalishaji, inayosababishwa na matumizi hafifu ya pembejeo bora (mbegu, mbolea, viuatilifu na zana bora za kilimo); kukosekana kwa muunganiko wa kiuzalishaji baina ya Wakulima, viwanda vya kukamua mafuta na watoa huduma za pembejeo na kifedha; uhaba wa teknolojia za kisasa za kukamua mafuta na mitaji ya kuwekeza katika kilimo na viwanda.

Aidha, mbali na changamoto hizo Waziri Mkuu Majaliwa amesema Serikali kupitia Wizara ya Kilimo imekuja na mikakati kadhaa. Mikakati hiyo ni pamoja na kuendelea kuwekeza katika Taasisi zinazohusika na utafiti na uzalishaji wa mbegu ili kuongeza tija.

“Kwa kuzingatia umuhimu wa mbegu bora; Serikali imeongeza bajeti ya Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) kutoka Shilingi bilioni 7.35 mwaka 2020/2021 hadi Shilingi bilioni 11.63 mwaka 2021/2022. Vilevile, bajeti ya Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA) imeongezeka kutoka bilioni 5.42 mwaka 2020/2021 hadi Shilingi bilioni 10.58 mwaka 2021/2022 ili kuongeza upatikanaji wa mbegu bora zikiwemo mbegu za mazao ya mafuta ya kula.” Amesisitiza Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

  • Google+
  • E-mail
  • PrintFriendly