WAZIRI MKUU ATEMBELEA SHAMBA NA KIWANDA CHA PARACHICHI RUNGWE
Awahamasisha wananchi Kuongezha mashamba kwasababu parachichi zina faida kubwa
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametembelea shamba la parachichi na kiwanda cha kuchakata mazao ya parachichi na kuwasisitiza wananchi walime zao hilo kwa kuwa faida yake ni kubwa.
Ametembelea shamba hilo leo (Jumapili, Agosti 1, 2021) katika kijiji cha Ilolo wilaya ya Rungwe, Mbeya na linamilikiwa na kampuni ya Kuza Africa na Moravian Farming PVT.
“Kilimo cha parachichi kina manufaa makubwa sana, wananchi ongezeni ukubwa wa mashamba ya parachichi na Serikali italisimamia kuanzia hatua za maandalizi ya shamba hadi masoko.”
Waziri Mkuu ameziagiza Halmashauri zote zinazolima zao la parachichi zianzishe vitalu vya kuotesha miche na kuigawa kwa wakulima ili kuhamasisha wananchi wengi kulima zao hilo.
Amesema zao la parachichi ni miongoni mwa mazao yenye faida kubwa na linazalishwa kwa gharama nafuu, hivyo amewahimiza wananchi kulima zao hilo kwa ajili ya kujikwamua kiuchumi.
Naye, Naibu Waziri wa Kilimo Hussein Bashe amewapongeza wawekezaji hao kwa kuwa wamewezesha wakulima kutatua changamoto ya soko la uhakika wa zao la parachichi.
Naibu Waziri huyo amesema mbali na kupatikana kwa soko la parachichi katika kiwanda hicho pia Serikali itahakikisha soko la parachichi za Tanzania nchini Afrika Kusini linafunguliwa.